Social Icons

Tuesday, December 11, 2012

VITUO VYA KULELEA WATOTO YATIMA WILAYANI MAKETE VYATAKIWA KUBUNI MIRADI ENDELEVU YA KUENDESHA VITUO HIVYO

Watoto yatima wanaoishi katika kituo cha Fema Matamba

Baadhi ya vitu alivyovitoa mkuu wa wilaya

Mkuu wa wilaya ya Makete Mh.Josephine Matiro(katikati) akisikiliza wimbo unaoimbwa na watoto wanaoishi kwenye kituo hicho(hawapo pichani), kulia kwake ni Askofu wa dayosisi ya kusini magharibi Job Mbwilo na kushoto ni Msimamizi wa kituo Bi Ala Mbwilo


Kituo cha watoto yatima cha FEMA Matamba

Watoto hao wakimuaga mkuu wa wilaya


 
 Na Edwin Moshi
 
 Vituo vinavyolelea watoto yatima wilayani Makete vimetakiwa kubuni na kuanzisha miradi endelevu itakayosaidia vituo hivyo kuzidi kutoa huduma bila kutegemea wahisani mbalimbali
Imeonekana kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia vituo hivyo kuendelea kuwepo hata kama wafadhili hao watasitisha ufadhili katika vituo hivyo, miradi waliyobuni na kuitekeleza itasaidia kuendesha vituo hivyo
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro wakati alipotembelea kituo cha watoto yatima cha Fema Matamba kwa lengo la kutoa msaada kwa watoto wanaolelewa kwenye kituo hicho
Amesema huu sio muda wa kubweteka na kuwategemea wafadhili pekee badala yake ni kuangalia mbele zaidi kwa kuanzisha miradi mbalimbali kama kilimo ambvyo itasaidia kuleta kipato cha vituo hivyo hasa ukizingatia hivi sasa wahisani wengi wanaanza kujitoa kufadhili masuala mbalimbali
“Sijui kwa nini sisi waafrika tunabweteka sana tunapenda sana misaada na kulalamika kazi hakuna wakati fursa tunazichezea wenyewe tu, sasa sijui tunataka nini, tuamke tutumie fursa tulizo nazo sasa” alisema
Hata hivyo mkuu huyo amepongeza uongozi wa kituo hicho kwa kuwa na moyo wa kusaidia kulea watoto hao yatima ambao mara nyingi jamii imewasahau, na kusema kuwa malipo ya kazi yao yatatolewa na mwenyezi MUNGU
Awali akitoa maelezo kuhusu kituo kwa Mh. Mkuuwa wilaya, msimamizi wa kituo hicho cha Fema Matamba Bi.Ala Mbwilo amesema kituo hicho kinategemea msaada wa wafadhili waliopo nje ya nchi ambao hutoa sh. Milioni 2 kila mwaka fedha ambazo bado hazitoshi kuendesha kituo hicho
Pamoja na hayo amesema ukosefua wa maji nalo ni tatizo lililopo eneo la Matamba ambalo huwalazimu kwenda mtoni kuchota maji ama kwenye bomba za vijiji jirani kwa ajili ya mahitaji ya kituo hicho
“Unajua mkuu watu huwa tunabweteka sana, hatutaki kulima wala kujishughulisha lakini tunapenda misaada tu, sasa misaada ikiisha tunakosa cha kufanya, tunabaki njia panda” alisema Bi. Mbwilo
Naye Askofu wa dayosisi ya kusini magharibi ambayo inamiliki kituo hicho Job Mbwilo ameshukuru kwa ujio huo wa mkuu wa wilaya huku akisema yeye ni kiongozi wa kwanza kufanya ziara ya kutembelea kituo hicho na kutoa msaada kwa watoto yatima wanaoishi hapo
Amesema wazo alilolitoa la kituo hicho kuwa na miradi endelevu watalifanyia kazi haraka iwezekanavyo kama namna ya kuboresha kituo hicho kwa kuwa jukumu la kuhakikisha watoto yatima popote duniani ni la jamii nzima, hivyo jamii nayo inapaswa kushirikiana kwa pamoja kuwalea watoto hao

1 comment:

  1. Tunashukuru ila tunaomba misaada hiyo ifanye kazi kwa walengwa.

    ReplyDelete